Kwa nini ziara ya Waziri wa Uingereza ni muhimu

Waziri wa Uingereza wa masuala ya Afrika, James Duddridge ameanza ziara yake nchini tangu jana kwa lengo la kuimarisha uhusiano kati ya nchi hizo mbili baada ya kuyumba kwa kipindi cha miaka sita iliyopita.

Dar es Salaam. Waziri wa Uingereza wa masuala ya Afrika, James Duddridge ameanza ziara yake nchini tangu jana kwa lengo la kuimarisha uhusiano kati ya nchi hizo mbili baada ya kuyumba kwa kipindi cha miaka sita iliyopita.

Taarifa iliyotolewa na Ubalozi wa Uingereza Dar es Salaam, imesema Duddridge atakuwa nchini kwa siku mbili ambazo atazitumia kufanya mikutano na viongozi wa kitaifa, akiwemo Rais Samia Suluhu Hassan na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Liberata Mulamula.

Pia atakutana na mawaziri kadhaa akiwemo Waziri wa Viwanda na Biashara, Kitila Mkumbo na Waziri wa Uwekezaji, Geoffrey Mwambe.

Siku ya pili anatarajiwa kwenda Zanzibar ambako atakutana na Rais Hussein Mwinyi na Makamu wa Kwanza wa Rais, Othman Masoud Othman.

Taarifa hiyo imemnukuu Duddridge akisema: “Natarajia kuwa na majadiliano na Rais na Serikali yake kwa ajili ya fursa za ushirikiano, ikiwa pamoja na kufanya kazi kwa pamoja katika sekta ya biashara na jinsi tutakavyopambana kwa pamoja na changamoto zikiwemo za mabadiliko ya tabianchi na maambukizi ya corona."

Ushirikiano baina ya nchi hizo mbili uliingia katika mishukosuko kwa miaka sita iliyopita, ambayo Uingereza ilikuwa inatoa matamko yaliyolenga kuirejesha Tanzania kwenye kile ambacho iliamini ni misingi ya utawala bora.

Kwa mfano, Duddridge mwenyewe alishatoa tamko la kukosoa uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 jinsi ulivyoendeshwa.

Alisema, ikiwa nchi inayoifadhili Tanzania kwa muda mrefu, Uingereza haikufurahishwa na kuwepo kwa malalamiko ya kuingiliwa kwa uchaguzi, ikiwa pamoja na kuingizwa kwa masanduku yaliyokuwa na kura kwenye vituo vya kupigia kura.

Alisema Uingereza pia haikufurahishwa na taarifa za vurugu na kuwekwa kwa polisi wengi katika uchaguzi huo, huku viongozi wa vyama vya upinzani wakikamatwa.

“Amani na mafanikio ya Tanzania yanahitaji mchakato bora wa demokra[1]sia ukiunganishwa na vyombo huru vya habari,” alisema